Shirika la habari la ABNA linaripoti kuwa: Serikali ya Gambia imewaachilia huru zaidi ya wafungwa 200, wakiwemo 31 waliofungwa kwa makosa ya uhaini kutokana na majaribio mbalimbali ya kumuangusha Rais Yahya Jammeh. Maelfu ya jamaa na marafiki walikusanyika nje ya gereza la Mile 2, katikati ya mji mkuu, Banjul, kuwalaki wapendwa wao mchana wa leo. Miongoni mwa walioachiwa huru, ni pamoja na wakuu wa zamani wa usalama wa taifa, sheria na polisi. Hata hivyo, wale waliotuhumiwa kuhusika na jaribio la mapinduzi la mwezi Disemba mwaka jana, wameendelea kubakia kizuizini, ingawa jamaa zao, akiwamo mama wa kiongozi wa mapinduzi hayo, wameachiwa. Baadhi ya wafungwa hao walikuwa wamekaa jela kwa zaidi ya miaka 15. Juzi Jumatano, Rais Jammeh alitangaza msamaha wa jumla, wakati akiadhimisha miaka 21 tangu aingie madarakani. Miongoni mwa wageni 49 walioachiwa huru ni raia watatu kutoka Uholanzi, Ujerumani na Australia, ambao walikuwa wamefungwa jela kwa makosa ya kukutwa na madawa ya kulevya.
Mwisho wa habari/ 291